Meza Fupa – Sehemu ya Tatu
Ilikuwa ni kawaida ya mji wetu inapofika usiku watu hawakuruhusiwa kuonekana wakizurura nje na ukionekana unaweza ukapewa adhabu yoyote ile. Miongoni mwa adhabu maarufu ilikuwa ni kuendeshwa kichura, kupigwa bakora, na kupelekwa gerezani iwapo utafanya ukaidi.
Nilikutana na askari waliokuwa wakifanya doria usiku waliojulikana kwa jina la ‘BANDIKABANDUA’. Walikuwa wanazunguka huku na kule na mimi nilijificha nyuma ya mti. Walipogeuka upande mwengine nilidamadama hadi kwenye nyumba moja ndogo. Huko nilimuona mtoto mdogo aliyetoka nje ya nyumba yao kufanya haja ndogo. Mlangoni alisimama mama yake akiwa anamsubiri mwanawe. Waliposikia chakarachakara za miguu yangu walishituka na mama yake yule mtoto alimuamrisha mwanawe arudi ndani.
Sikuwa na msaada wowote kwa sababu watu wengi waliamini kuwa ukoo wetu ndio serikali yenyewe kwa hiyo hawakutupend. Kibaya zaidi nilichokihofia ni kugundulikana tena nikiwa hai. Nikaamua kufuata njia iliyoelekea bondeni. Mwangaza wa tochi ulinishitua na kunifanya nijibanze sehemu ambayo sitoweza kuonekana. Lakini ilinibidi nipige ukelele pale nilipopata maumivu makali mguuni baada ya kutafunwa na tandu.
Aliyemulika tochi alikuwa ni askari wa doria wa kikosi cha ‘BANDIKABANDUA’ na alikuja hadi nilipokuwa. Nilijibana ili sauti yangu isisikike lakini aliweza kuniona na kunimulika usoni. Yule kijana alinitaka nisiwe na wasi wasi baada ya kubaini kuwa aliyemuona alikuwa ni mtu aliyemfahamu. Alinifahamu kwa sababu alikuwa akija sana nyumbani alipokuwa na maagizo yoyote yaliyomuhusu baba, na siku nyingi alikuwa ananiwinda kama sala na chui. Alikuwa ananipenda sana lakini baba yangu alikuwa ni waziri wake kwa hiyo alikuwa mwoga. Aliniambia kuwa nipo hatarini kwani nimetafutwa sana bila ya kuonekana baada ya familia yangu yote kuuawa isipokuwa mimi ambaye kwa muda wote sikuwepo nyumbani. Askari huyu aliitwa Tafakari. Alinitaka nistahamili kwa mitihani ile na aliniahidi kuwa na mimi bega kwa bega. Askari wenzake walianza kumpigia kelele baada ya kuona kuwa amechukuwa muda mkubwa bila ya kurudi. Aliponiuliza sehemu niliyokuwa nikielekea sikuwa na jibu. Tafakari hakuweza kuendelea na mazungumzo yoyote kwa sababu askari wenzake walikuwa wameshafika. Nikaamua kumuacha akiwa anawababaisha wasiendelee kuja upande niliokuwepo mimi. Niliendelea kutokomea bondeni.
Ulikuwa ni usiku wa kiza lakini nilikwenda mwendo mkubwa nikikata kwenye mabonde nisiyoyajua. Nilipofika sehemu ambayo nilihisi kuwa ninaweza nikapata usalama na utulivu nilitulia. Ilikuwa ni chini ya mti mkubwa. Niliweka begi langu chini, nikatandika kanga yangu na kulala. Sikuweza kuupata usingizi, nilijifikiria na kujiuliza kuwa nitaendelea kuishi katika hali ile hadi muda gani! Nilifikiria kujinyonga lakini niliona kuwa ni upumbavu kujidhulumu nafsi yangu kwa sababu ya mitihani ya kidunia
Ilipokaribia alfajiri, kwa mbali nilihisi usingizi na nikalala usingizi mzito. Sikuchukuwa muda mkubwa niliamshwa na mbwa waliokuwa wakifukuzana, waliniruka na kuendelea safari yao. Jua lilianza kuchomoza na kuisabahi dunia. Tafakari alinitafuta kubaini wapi nilielekea usiku ule. Alikuja hadi bonde nililojificha. Nilikuwa ninaosha uso wangu katika chemchem moja ya maji iliyokuwepo msituni, punde nilimuona kijana mmoja akiangaza angaza huku na kule kama aliyekuwa anatafuta kitu. Nilijficha nikiamini kuwa ni askari waliotumwa kunitafuta mimi.
Tafakari aliniona na ndipo alipoamua kunifuata. Nilipomuona huyo kijana ananijia nilijuwa kuwa huo ulikuwa mwisho wangu. Nililitupa begi langu ili niwe mwepesi wa kukimbia. Lakini kila nilipokuwa nikiangalia nyuma nilimuona mtu ananifukuza kwa mwendo wa kasi na nilishangaa zaidi pale aliponiita kwa jina langu. Niligeuka na kumtambua kuwa alikuwa Tafakari. Huyu nilimuamini, nilijua kuwa hawezi kuwa mbaya wangu. Usiku uliopita aliweza kuniokoa katika wakati mgumu. Tafakari alinipatia begi langu nililolidondosha na alinitaka nikae tuzungumze.
” Sikiliza Msiri, najua upo katika wakati mgumu unaohitaji subira ya hali ya juu, na siku zote anayekusaidia kwenye matatizo kwa moyo safi, huyo ndiye akupendae, kwa hiyo ujuwe kuwa nipo tayari kukusaidia, ila na wewe unisaidie!”
Sentensi hii ya mwisho ilinipa utata kidogo, nilitaka aweke bayana namna gani anataka nimsaide.
“ Kwani wewe Msiri hujui kuwa mimi siku nyingi nakuwinda lakini nakuwinda kwa malengo, ninataka kukuoa lakini wakati baba yako yuko hai sikuweza kufanya hayo kutokana na hadhi ya familia yako”
Sikuweza kutoa jibu kwa wakati ule badala yake nilimtaka anipe muda , nilikuwa nimechanganyikiwa, sina pa kuelekea. Alitaka niendelee kustahamili anipeleke kijiji cha jirani nikapate nusura kwa baadhi ya ndugu zake walioishi huko.
Yalikuwa ni masafa marefu kutoka bonde lile hadi kijijini. Tafakari alinipeleka kwa mama yake mdogo. Tulipofika aliwaeleza hali halisi lakini wote wakagoma kunipa hifadhi kwa kuhofia kuuwawa iwapo watajulikana kuwa wamemficha mtu aliyekuwa anatafutwa na serikali. Alikuwepo mtoto mdogo wa miaka kumi na tatu ambaye alinihurumia sana kusikia mkasa wangu. Aliwataka wazee wake wanisaidie kuishi pale kwani sehemu ile ilikuwa nje ya mji kidogo kwa hiyo ni mara chache sana kuwaona maafisa wa serikali wakija maeneo yale.
Walikubali niishi nao na Tafakari aliahidi kunipa taarifa zote kwa kile kilichokuwa kinaendelea mjini.
Alikuwa na kawaida ya kunitembelea kila mwisho wa wiki na kuniletea zawadi na vyakula. Niliishi vizuri pale na kujihisi kama nipo nyumbani, sikupenda kutembea sana kwa kuhofia kuonekana na watu walioweza kunifahamu, niliishi siku nyingi na hakuna aliyejua taarifa zangu. Mwanzo nilikuwa na mawazo mengi kuhusu wazee wangu lakini niliizoea hali ile na nikaisahau kabisa.
Miaka ilipita, Tafakari aliamua kunioa lakini aliuliwa baada ya kushambuliwa na wananchi waliokuwa na hasira. Tafakari alikuwa katika kazi yake ya doria yeye na wenzake lakini walivamiwa na vijana waliokuwa na hasira kwa kukamatwa rafiki yao aliyekuwa akizurura usiku. Vijana hao waliwavamia askari na kuwashambulia, mume wangu alipigwa chupa ya kichwa, vigae vilibaki kichwani, alipoteza damu nyingi na kupoteza maisha. Huo ulikuwa msiba mkubwa sana kwangu.
Baada ya uyatima nilioupata miaka ya nyuma sasa nikawa kizuka. Maisha yalikwenda hivyo hivyo na kwa bahati mbaya sikupata mtoto.