Meza Fupa Sehemu Ya 4
Meza Fupa – Sehemu ya Nne
Ilipoishia: “Baada ya uyatima nilioupata miaka ya nyuma sasa ni kizuka, maisha yalikwenda hivyo hivyo na kwa bahati mbaya sikupata mtoto…..” Sasa endelea….
“Baada ya miaka mingi kupita niliamua kwenda mjini kutembea na mama yake mdogo Tafakari, tulipanda gari za abiria, siku niliyofika tu mjini nilikamatwa na askari bila ya kujua ni wakati gani wamejua kuwa nipo mjini, na sikuwa na wasiwasi sana kwa sababu nilijuwa kuwa itakuwa vigumu kuitambua sura yangu.
“Sasa nilijua kuwa ulikuwa ndio mwisho wa maisha yangu, nilipelekwa katika nyumba moja kubwa sana, walikuwemo vijana wengi wa rika yangu, wanaume na wanawake. Baadhi ya vijana niliweza kuwajua lakini wengine ilikuwa vigumu.
“Nilikaa gerezani kwa muda wa miaka mitano, baada ya kutoka gerezani niliamua kurudi kule kule kijijini, niliwataka vijana wanisaidie kujenga bondeni, sikujua ni kitu gani lakini moyo wangu ulitamani sana niishi maisha ya upweke, nilikaa mbali na watu.
“Kadiri siku zilivyokwenda na watu tulizidi kuwazika, niliishi bondeni kule nikiyaendeleza mashamba waliyoyaacha jamaa zake Tafakari, mimi ndiye niliyekuwa msimamizi wa mashamba kwa wakati huu. Aliyezaliwa na kukuwa pia aliweza kunikuta bado naishi pasipokujua historia yangu. Nilikuwa na ndoto za mabadiliko siku nyingi, nilipata kuzihifadhi nyaraka na majalada ya zamani sana ya siri aliyokuwa nayo baba yangu.
“Niliingia ndani na kuwaonesha jalada moja kubwa sana, lilikuwa limechakaa sana na kurasa nyengine zilikuwa zimeshachanika.
“Lilikuwa linaonesha historia na asili ya viongozi waliotawala nchi ile, ilikuwepo barua ya siri ya kutaka kutoa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi kuwapa nchi jirani ambao walikuwa na utajiri wa mafuta, viongozi wetu walikuwa wako tayari wageni ndio watawale na wao waweze kumiliki sehemu ya pato la mafuta ambalo litaingia kwenye mifuko yao binafsi.
“Hii ilikuwa ni ajenda ya siri waliyokuwa nayo viongozi wa miaka hiyo au niseme karne iliyopita, walikuwa wako tayari kuishi nje ya nchi na wageni watawale, nilikuwa sijui kuna kitu gani kinachowavutia hawa wageni wakati sikupata kusikia kuwa kuna rasilimali adhimu kama walizo nazo wao.
“Nikawaonesha jalada jengine lililoandikwa siri nyengine linaloonesha mafanikio ya mpango wao wa kuwaacha wageni watawale kwa dhamira ya kupata sehemu ya pato la rasilimali ya mafuta. Pia ilikuwepo orodha ya watu ambao wapo ndani ya nchi yetu na ndio viongozi wetu lakini asili yao ni nchi jirani ila walipata madaraka ya kutuongoza kwa sababu tu wamekubaliana na viongozi wetu kama lilivyoonesha jalada la kwanza.”
Bi Msiri akamaliza simulizi yake refu na Miftaha na wenziwe wakabaki midomo wazi. Butwaa limewashika baada ya kuelezwa mambo ambayo hawajawahi kuyasikia tangu walipozaliwa. Bi Msiri akawataka wayajue yale na kuyafanyia kazi.
“Kumbe ndio maana baadhi ya viongozi wametuwekea kisu cha shingo kwa sababu si wetu, mh! Kwa sababu miye nijuwavyo ni kuwa zimwi likujuwalo halikuli likakwisha, lakini hawa wanatumeza haswaa,” alisema Maimuna baada ya kujionea mambo ambayo hakuyajua kabla.
Miftaha alimshukuru sana Bi Msiri aliyekuwa anazungumza kwa hisia kali huku machozi yakibubujika machoni mwake, alisema kuwa akili yake haijapata kugonjwa hata siku moja, alikuwa na fahamu yake ya kila lililotokea, aliwasisitiza Miftaha na wenzake kwa kuwataka waamke kama bado hawajaamka.
Alisema kuwa yeye hakuwa na muda mrefu atakufa, lakini hamu yake ni kuupanda mche ambao watakuja kufaidi matunda yake vizazi vijavyo, ila ni nani ataijua historia ya kweli kama itafichwa na wanaoificha watapotea? Sasa wao ndio wasimamizi wa yale.
Baada ya hapo Bi Msiri alimtaka Miftaha afanye mpango katika mkutano unaosemekana kufanyika mwezi ujao apate nafasi ya kuonesha umalenga wake kwa sababu alikuwa na ujumbe maalum aliotaka kuufikisha kwa jamii. Ulikuwa ni mkutano wa serikali na mara nyingi mratibu wa mambo haya alikuwa ni mshauri wa raisi ambaye ni baba yake Miftaha. Miftaha aliahidi kulisimamia hilo kwa kumshawishi baba yake ili bi Msiri aje atoe alilolikusudia.
Vijana wale walitoa pesa kumpa Bi Msiri kwa kazi kubwa aliyoifanya.
“Nyinyi watoto kumbe ndio wale wale eeenh! Sasa pesa hizi za nini? Mnanipa rushwa sio? Eenh! Sitaki ujinga nyinyi watoto amkeni tujenge taifa.”
Miftaha na wenzake wakaomba radhi na kusema kuwa halikuwa lengo lao ila ni zawadi tu waliomletea.
Waliaga na kuondoka.
Kazi ilikuwa kwa Miftaha ambaye alitakiwa amshawishi baba yake katika sehemu ya kutumbuiza kabla ya kuhutubia raisi apatiwe nafasi Bi Msiri, bibi aliyeishi miaka mingi kuliko sana kuliko kawaida, kuja kughani tungo yake.
Alifanikiwa na kutakiwa ahakikishe kuwa ujumbe atakaoufikisha Bi Msiri uwe unaendana na matakwa ya utawala. Alikubali hivyo akiwa na yakini kuwa Bi Msiri alikusudia kufikisha ujumbe ambao watu wa utawala wasingeupenda.
Siku iliwadia, Bi Msiri alipewa taarifa na kutakiwa ajiandae kwa ajili ya kazi yake aliyoikusudia.
“Sifikirii kuwa nina haja ya kujiandaa, miaka mia mbili ni shuhuda wa maandalizi yangu,” alisema Bi Msiri kwa kujiamini.