Sehemu ya kwanza

Hadithi ya Meza Fupa – Sehemu ya Kwanza

kibibiBILA ya kubaini, chembe ndogo ya wema uipandayo ardhini, huenda Ikachipua na kutoa mti mkubwa utakaoweza kukupatia kivuli au kuwapatia wengine wakati wa jua kali la kiangazi.

Ilikuwa ni safari ya mwendo mkubwa, walikuwa ni vijana watatu walioongozana katika kukitafuta kijiji ambacho walipata kusikia kuwa aliishi bibi mwenye historia nzima ya nchi yao. Bibi aliyeishi miaka mia mbili, ndie pekeye aliyeweza kutambua hali halisi ya nchi yao, sio kama haikuwepo historia, lakini historia iliyokuwepo ilipotoshwa na kuwaziba macho vijana waitwao kizazi kipya.

Na Ally HilalNa Ally Hilal

Walilkuwa ni vijana watatu wenye umri kati ya miaka ishirini hadi thelathini. Aliyekuwa mstari wa mbele katika kuiandaa safari hi alikuwa ni Miftaha, kijana jasiri asiyeogopa kitu katika kuitafuta haki. Mwili wake ulionekana dhaifu kutokana na wembamba wake, alikuwa ni mweusi kidogo, hakuwa mrefu sana ila wembamba wa umbile lake ulimfanya aonekane mrefu wa kimo.

Wengine walikuwa ni Suheli na Maimuna. Wanaume wawili na mwanamke mmoja, Maimuna alikuwa ni ndugu yake Miftaha.

Bi. Msiri alifanana na jina lake, moyo wake uliyabeba mengi tena makubwa mithili ya dunia au sawa na umri wake, miaka mia mbili kwa ulimwengu wa sasa utatolewa kwenye vyombo vya habari na kuingizwa katika kundi la watu wa maajabu. Huu ndio ulikuwa umri wa bibi huyu aliyeishi katika kiijiji cha Maukio. Pamoja na umri wake mkubwa, bibi huyu alikuwa na meno yote thelathni na mbili, macho yake yalikuwa hayaoni tena vizuri lakini alikuwa na uwezo wa kusikia kama mtoto mdogo, si rahisi kumsengenya ukiwa karibu yake.

Alikuwa anatembea kwa tabu sana, alitembea kwa mkongojo wake uliochongwa vizuri, ulichorwa nakshi  nzuri za msumeno na ulikuwa umeandikwa TUTAFIKAJE?

Bibi huyu aliishi kando na mto mkubwa uliokuwepo katika bonde kubwa kijijini pale, maisha yake yalikuwa ya upweke tangu alipokuwa na miaka ishirini baada ya kuipoteza familia yake yote katika hali tata hadi leo hakuweza kuwaona tena.

Alikuwa mtu wa mwanzo kuhamia kijiji hiki baada ya kukimbia mjini kwao na kujitokomeza katika bonde hili, aliishi kwa tabu sana akiwa mafichoni huku ambako kulikuwa mbali na mji aliotoka.

Miaka ilivyozidi kusonga mbele, nyumba zilisogea hadi kufika sehemu aliyoishi Bi Msiri. Ni historia ndefu ambayo hakuna aliyeijua, walioishi naye walikuwa hawajui chochote kuhusu bibi huyu, walimuona kuwa ni bibi wa kawaida tu asiyepungua umri wa miaka themanini kutokana na muonekano wake lakini hawakuujua umri halisi wa bibi huyu.

Hakuwahi kuwa na rafiki wa karibu ambaye aliweza kubadilishana naye mawazo zaidi ya bi Tausi aliyekuwa mkulima katika bonde hili, alikuwa na shamba lake mwenyewe.

Linaweza likajengeka suali katika akili ya mtu kuhusu bibi huyu aliyejitenga na watu kwa miaka mingi na aliyebeba siri nzito moyoni mwake, suali jengine ni kuwa vipi Miftaha na wenzake waliujuwa uwepo wa bibi huyu na kwa ajili gani waliamua kumtafuta.

Miftaha ni miongoni mwa vijana waliopata elimu, alisoma hadi chuo kikuu nje ya nchi, alibahatika kusomeshwa na serikali yake iliyokuwa madarakani kutokana na nafasi ya baba yake, baba yake alikuwa mfuasi mkubwa wa chama kilichokuwepo madarakani, hapakuwa na chama cha upinzani kwa sababu serikali iliogopa kupingwa na kukosa wafuasi iwapo wataendesha serikali yao kinyume na wanavyotaka wananchi.

Pamoja na hayo wananchi wengi hawakukiunga mkono chama hiki, walikipinga chini kwa chini kwa kuhofia kukamatwa na kuishia gerezani. Pamoja na kwamba Miftaha aliishi kwa baba yake, baba yake alikuwa ni mshauri wa raisi wa nchi, aliyajua mengi yaliyokuwa yakitendeka nchini, lakini watoto wake wote wawili hawakukubaliana naye, kila siku waligombana na baba yao.

Licha ya elimu yake, Miftaha hakuweza kupata nafasi za juu serikalini kama ilivyokusudiwa na baba yake hapo awali, kusoma kwake nje ilikuwa ni kuandaliwa ili aweze kuingizwa katika mfumo wa serikali lakini alionekana na msimamo tofauti, kutokana na sababu hiyo alibaki kuwa mwalimu wa skuli.

Siku moja alirudi mapema skuli kwa sababu kichwa kilikuwa kinamuuma, ilikuwa ni jioni saa kumi na moja kamili, alikutana na Bibi mmoja aliyechoka sana, mguu wake ulikuwa unavuja damu, alikuwa ametafunwa na nyoka, ilikuwepo gari moja tu inayokuja kutoka kijiji alichoishi bibi huyu, ilikuja asubuhi na kuondoka jioni, alikuwa ni Bi Tausi, rafiki yake bi Msiri.

Miftaha alisimama na kusogea pembeni alipokuwepo bibi huyu, alimuweka kwenye kibao cha baiskeli yake na kumpeleka hospitali.

Hakuna aliyemjali mgonjwa, kila mmoja alijishuhulisha na kazi zake, baadhi ya wauguzi walimtazama mgonjwa wa Miftaha kwa dharau bila ya kujali kuwa alikuwa katika hali mbaya kwani sumu ya nyoka ilikuwa inazidi kumuenea mwilini. Daktari wa zamu alikuwa amekaa nje anasoma kitabu cha riwaya. Miftaha alitoka hadi nje baada ya kuambiwa kuwa daktari wa zamu alikuwepo nje, alimkuta daktari amewacha kitabu na sasa anacheza karata na vijana wa mtaa. Ilimuuma sana kumuona daktari anacheza karata huku wagonjwa wakiumia bila ya matibabu, alimsogelea daktari na kumwambia kuwa kuna mgonjwa yuko hali mbaya.

Alipata majibu ya kukatisha tama.

“Kijana mimi mwenyewe ni mgonjwa hapa, au hujui kama na sisi madaktari ni wagonjwa na tiba yetu hatujaiona, vilio vyetu havisikilikani maana tuna sauti ndogo, ila nyinyi munataka tuvisikilize vilio vyenu, je vyetu avisikilize nani?

Maneno haya alikuwa anayazungumza daktari kumwambia Miftaha bila ya kumtazama aliyekuwa akizungumza naye.

“Kwa hiyo unataka kunambia kuwa wagonjwa wetu tuwaache wafe?”

Yule daktari aliendelea kucheza karata na kumjibu Miftaha bila ya kumtazama usoni.

“Kufa! Mh! Sasa wewe unafikiri mimi unayeniita daktari niko hai! Kwa lipi la kusema ni uhai, mimi ni maiti kwenenda!”

Login
Users Online