Meza Fupa – Sehemu ya Pili

Meza Fupa – Sehemu ya Pili

kibibiWALIPOFIKA ndani alianza kuchukuwa jina la mgonjwa na maelezo mafupi, baada ya hapo alimchoma sindano ya kuondosha sumu ile lakini ilikuwa imeshaenea mwili mzima. Bi Tausi alijiona kuwa hawezi kuendelea kuishi, alimuomba daktari amruhusu Mwalimu Miftaha apite ndani kwani kulikuwa kitu akitaka kumwambia. Daktari aliomba apewe yeye ule ujumbe aufikishe kwa Miftaha lakini Bi Tausi alikataa katakata, akidai kuwa ‘kuagiza n’maviza’

Mwalimu Miftaha aliruhusiwa apite ndani kumsikiliza Bi Tausi; naye Bi Tausi alimtaka daktari asubiri nje mara moja ili azungumze na Miftaha.

“ Mwanangu, ahsante, miye naishi kijiji cha Maukioni, nnakuja n’jini kutimiza utumwa wa shoga yangu aliyenileta huku, ni mzee sana tena wa miaka mingi, kutokana na hali yake, basi hawezi kuishi siku nyingi na… na…”

Alikohoa na kuugua kwa  maumivu na baadaye akaendelea:

“Kanituma nintafutie kijana mwenye mapenzi na nchi hii ambaye ana dira nzuri ya maisha yake lakini sijamuona, nlikuwa narudi bila ya mafanikio na ndio maana baada ya kukuona weye nahisi unanifaa, nenda kwa huyu  bibi ana kitu cha kukwambia, aitwa Bi Msiri”

Na Ally HilalNa Ally Hilal

Alikohoa na kuvuta pumzi yake ya mwisho na hapo ndipo alipoaga dunia.

Miftaha aliumia sana, alimwita daktari kumuangalia mgonjwa wake lakini alikuwa ameshapoteza maisha.

Alirudi nyumbani kwao na kuchukuwa farasi wake, aliupakia mwili wa marehemu na kuupeleka kijiji cha Maukioni, alifika kjijini hapo saa mbili usiku. Aliwaulizia ndugu wa bibi yule na kuwapata. Baada ya kuwakabidhi maiti wao aliwaaeleza yote yaliyomkuta bibi yule halafu aliaga na kuahidi kurudi baada ya siku mbili.

Baada ya siku mbili, aliamua kwenda kijiji cha Maukioni pamoja na wenzake wawili, dada yake aliyeitwa Maimuna na mwalimu mwenzake aliyeitwa Suheli.

Ilikuwa ni asubuhi mapema, vijana hawa walielekea kijijini kumtafuta Bi Msiri. Walikuwa na farasi wawili, mmoja alipanda Miftaha na Maimuna na mwengine alipanda Suheli.

Walifikia nyumbani kwa Bi Tausi ambaye alizikwa siku moja kabla, walikaa matangani kwa muda wa masaa mawili, walikaribishwa vizuri sana na wenyeji wao. Baada ya hapo waliomba wafahamishwe sehemu aliyokuwa akiishi Bi Msiri. Kijana mmoja mdogo aliyekuwa akianika nguo, alitakiwa awapeleke bondeni ilipokuwepo nyumba ya bibi huyu.

Ilikuwa ni kibanda kidogo kilichoezekwa kwa makuti, baadhi ya sehemu kilizibwa kwa makuti, nje alikuwepo bibi anatwanga unga wa muhogo. Alikuwa amekaa kwenye gogo la mnazi, alivaa nguo zilizochakaa sana. Kanga yake iliandikwa “NIMESTAHAMILI TABU KUPATA SI AJABU”

Ujumbe huu ulimfanya Miftaha atabasamu peke yake, walisogea alipokuwepo Bi Msiri na kumsalimia.

“Shikamoo bibi”

Bi Msiri alikuwa haoni vizuri lakini aliweza kusikia vizuri, aliwaitikia na kuwauliza maswali mengi.

“Marahaba wanangu, sijawajua nnani nyiyee! Macho yenyewe yan’kwisha zake, sioni taaaa ule n’kono wangu.”

Miftaha alijitambulisha kwa kutoa mkasa wa Bi Tausi.  Bi Msiri alisikitika sana alipotajiwa shoga yake mpenzi aliyepoteza maisha siku mbili tu zilizopita, aliwachangamkia wageni wake baada ya kubaini kuwa ndio waliouleta mwili wa marehemu. Aliumia sana kwa sababu safari ya Bi Tausi kwenda mjini ilikuwa ni kutekeleza agizo lake Bi Msiri aliyemtaka akamtafutie mtu mwenye uchungu wa nchi yake, mzalendo wa kweli na si wa kinafiki. Baada ya kushindwa kutimiza lengo lake aliamua kurudi kijijini kwao na hapo ndipo yakamfika matatizo. Hiyo ndiyo iliyokuwa sababu ya kifo chake.

Bi Msiri aliwakaribisha chini ya mwembe na kuwatandikia mkeka.  Bibi huyu alikuwa malenga mzuri sana, alizungumza maneno kwa ufupi sana lakini yalibeba maana nzito, Kiswahili chake kilimfurahisha sana Miftaha.

************************

“Wanangu natakalitema fupa, nimelimeza likanikwama, hakuna anayejua lakini n’taka wajuvya nyiye, naamini mumetoka kwenye udongo wenye rutuba nzuri, ingawa maji machafu huuathiri udongo wenu lakini naamini kuwa bado kuna michirizi ya maji safi ipitayo kwenye udongo huo, pia hewa safi kutokea pande za janibu ya kaskazini na kusini yake zaweza ipunguza sumu hii ya hatari.

“Nimeona kuwa kumeza fupa si suluhu ya kunifanya nisiwe na njaa tena, wala si sababu ya kuwatia njaa mbwa wanaohaha huku na kule kwa kulitafuta fupa. Nataka mujuwe wanangu kuwa mimi nimekula chumvi sana. Hakuna anayejua hata mmoja kuwa mimi nimepindukia na kupindukia kuishi, nayajua hayo wasiyoyajua mababu wa babu zenu, katika wahenga na miye nimo na n’shahengeka. Nayajua hayo meusi yaitwayo meupe na meupe yaitwayo kijani. Umri wangu unapotea sasa, hebu tulieni niwajuvye.

“Nina miaka mia mbili, na nimeishi kijijiini hapa tangu baada ya baba yangu kuuwawa na familia yangu yote isipokuwa mimi.

“Mimi peke yangu nilisalimika, nilikosa bahati kwetu, wazazi wangu walinifanya kama mtoto waliyeniokota. Nyumbani kwetu alikuwepo mfanyakazi, nilimhurumia sana kwa kazi nyingi alizokuwa nazo, hili liliwakera wazazi, na kwa vile nilikosa bahati walizidi kulifanya hili kama kosa la jinai. Niliambiwa kuwa kuanzia wakati huo nitakuwa mfanyakazi wa ndani na yule mfanyakazi alifukuzwa nyumbani. Maisha yangu yalikuwa magumu pamoja na kuwa niliishi na wazee wangu tena hawakuwa na maisha magumu. Baba yangu  alikuwa waziri wa ardhi na majengo.

“Siku moja, nilitoka kuelekea mtoni kufua kama ilivyokuwa kawaida yangu. Nilikusanyiwa nguo za nyumba nzima, sijawahi kulalamika hata siku moja, nilizifua nguo zote.

“Baada ya kumaliza nilirudi nyumbani na kumkuta mama yangu kwenye mlango wa jikoni akiwa ameshafariki, alikuwa anavuja damu kichwani. Nilipoingia ndani niliwakuta ndugu zangu wawili wa miaka kumi na tano wameshafariki, hawa walikuwa pacha, nilichanganyikiwa na kuanza kuita kwa sauti kubwa iliyojaa kitetemeshi. Hakuna aliyeitika, nililia sana, niliamua kuingia chumbani kwa baba ambako moyo wangu ulizidi kushituka nilipomkuta baba yangu amelala kitandani, kichwa chake kilikuwa kinaninginia chini na miguu ilikuwepo kitandani.  Alikuwa amekatwa katwa mkono wake na kichwa chake kilivuja damu nyingi.

“Sikujua nifanye nini, nilikuwa na maswali mengi ya kujiuliza kuhusiana na aliyefanya mauji yale ya kutisha. Nilibaini baada ya kuokota kitambulisho chenye picha ya mtu.  Kilikuwa ni kitambulisho cha afisa wa polisi kilichokuwepo sakafuni, pia kilikuwepo kipochi mlangoni. Nilikifungua na kukuta makaratasi mengi, nilipojaribu kukifungua kikaratasi kimoja niliona kimeandikwa jina la afisa yule yule. Baada ya dakika mbili nikiwa nimezubaa pasipokujua cha kufanya, nilisikia mvumo wa gari nje ya nyumba yetu. Nilijificha mvunguni mwa kitanda cha baba. Niliweza kuviona viatu vya buti nyeusi.  Nilitamani niione sura yake lakini sikuweza kuiona kwa wakati ule.

Nilisikia sauti mbili zikijinadi na kusema bila woga.

“Pochi yangu na kitambulisho hivi hapa”

Yule mwengine akajibu:

“Mawaziri kama hawa tunafyeka sisi, hawatuyumbishi, hivi unaijua sababu ya kuteketea kwa hili jamaa?”

Aliuliza yule askari.

“Najua, huyu juzi alisema kuwa raisi inabidi abadilike asiburuzwe na matakwa yake kwani yeye amewekwa na wananchi”

“Ah! Kumbe wewe wajua hivyo tu! Huna ujualo”

Walianza kubishana, niliroa jasho na miguu ilinitetemeka huku masikio yangu yakisikiliza zile sauti.

“Wewe hujui, huyu jamaa amepewa usimamizi wa ardhi, ameamua kuwatafuta wananchi wenye umiliki halali wa eka zao na wengine amefanikiwa kuwarudishia eka zao za mashamba na hayo mengine yamefuatia juu tu, na sasa wameamua kuuziba huu mdomo”

“Haya yote niliyasikia, nilifanya kuchungulia kidogo nikaweza kuziona sura zao. Alikuwa ni afisa wa polisi pamoja na waziri ambaye alikuwa anakuja sana nyumbani, alikuwa ni rafiki wa karibu sana na baba yangu Ama kweli kikulacho kinguoni mwako, waziri huyu huyu ndiye aliyemuahidi baba kuwa hamu yake ni kuona familia yetu na familia yao zinazidi kuungana kupitia  ndoa za watoto wao, yaani mimi na mtoto wake waziri huyu.

“Baada ya muda walitoka nje na kuondoka. Nilijifungia chumba cha mabandani hadi usiku na nikaondoka. Nilikuwa nikizisikia sauti za watu waliokuwa wakiingia na kutoka.

“Ilipofika usiku nilitoka na kuelekea chumba cha marehemu baba yangu, mwili wake ulikuwa umeshaondoshwa, na hata miili ya mama na wadogo zangu haikuwepo tena. Iliniuma sana, nilichukuwa begi langu la nguo na kuondoka nikiwa sijui ninapokwenda.  Waswahili wanasema “Kua uone mambo!”

Sehemu ya Nne